Suala la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM),
Vicky Kamata limechukua sura mpya baada ya mzazi mwenza wa mchumba wa
mbunge huyo, kukanusha taarifa kwamba alikwenda Dodoma kwa lengo la
kuomba msaada kwa viongozi wa Bunge.
Kauli ya mama huyo imezidisha utata
katika sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa hiyo iliyokuwa ifanyike
Jumamosi baada ya kutokea habari kuwa mwanamke mmoja alikwenda bungeni
mjini Dodoma kutaka kuonana na Spika kwa lengo la kuomba Bunge limsaidie
kupata haki yake kabla ya harusi hiyo kufungwa na hivyo kusababisha
harusi kutofanyika.
Vicky Kamata, ambaye alijizolea umaarufu kutokana na wimbo wake wa “Wanawake na Maendeleo” na
baadaye kuingia bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2010, alikuwa afunge
ndoa na mtu aitwaye Charles Gardiner Jumamosi iliyopita jijini Dar es
Salaam, lakini haikufanyika .
Jana, Kinavi Dadi, ambaye ni mzazi mwenza wa Gardiner, alikanusha kufunga safari hadi Dodoma kwa lengo hilo.
“Ni kweli kwamba Charles ni baba
watoto wangu, lakini sijawahi kwenda Dodoma na wala sifahamu chochote
kuhusu safari hiyo. Nadhani inatosha,” alisema mama huyo na hakutaka
mazungumzo zaidi.
Baadaye kidogo mmoja wa ndugu wa Kinavi,
ambaye aliomba asitajwe jina lake, alikiri ndugu yao kufunga ndoa na
Gardiner Juni 2004 na kujaliwa kupata watoto wawili, lakini
walitofautiana na baadaye ndoa yao kuvunjwa mwaka 2012.
Alisema taarifa kwamba aliyepata kuwa
mke wa Gardiner alikwenda Dodoma kuomba msaada wa Bunge zimewaumiza sana
kama familia kutokana na ukweli kwamba Kinavi ndiye anayefahamika kuwa
mke wa kwanza.
Bungeni Dodoma
Wakati hayo yakiendelea, habari kutoka bungeni Dodoma zinasema mwanamke aliyedaiwa kuwa mke wa Gardiner ni‘feki’ na alikuwa wa kutengenezwa na baadhi ya wabunge kwa lengo la kumtibulia Vicky Kamata.
Mpango huo unadaiwa kuwahusisha wabunge
wanawake wanne; watatu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka
Chadema ambao awali waliapa kwamba ndoa ya mbunge mwenzao isingefungwa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, waandishi
wetu waliopo Dodoma walimsaka mwanamama huyo bila mafanikio na baadaye
waliambiwa kwamba haikuwa rahisi kumwona kwani hakuwa halisi.
Kundi la wabunge hao ndilo lilimwingiza
mwanamke huyo katika viwanja vya Bunge kwa lengo la kumkutanisha na
viongozi wa taasisi hiyo, lakini mpango huo ulishindikana.
Mwishoni mwa wiki, Naibu Spika Job
Ndugai alisema anakumbuka kwamba alipewa taarifa za kuwapo kwa mwanamke
anayemtafuta, lakini hadi alipoondoka kwenda jimboni kwake Kongwa hakuwa
ameonana naye.
Juzi Kamata aliliambia Mwananchi kwamba
naye alisikia taarifa za kuwapo kwa mwanamke huyo mjini Dodoma, lakini
hakuweza kufahamu ni nani kutokana na kwamba alikuwa bado amelazwa
hospitalini.
Mbunge huyo alilazwa kwa siku sita
katika Hospitali ya Tabata General, iliyopo Segerea, Dar es Salaam na
aliruhusiwa juzi. Anatarajia kwenda Dodoma wakati wowote.
Mapenzi ya Mungu
Mbunge huyo juzi alizungumzia kutofungwa kwa ndoa yake na kusema anaamini kilichotokea “ni mapenzi ya Mungu”.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake,
Sinza jijini Dar es Salaam, Kamata alisema ingawa ndoa hiyo
haijafungwa, moyo wake una amani kwa kuwa alimwomba Mungu kuhusu suala
hilo kwa muda mrefu na hicho ndicho Mungu alichojibu.
Kamata alisema licha ya kuwa tukio la
kutokufungwa kwa ndoa hiyo kuwa zito na ambalo lingeweza kumjeruhi moyo,
amekuwa na amani tofauti na ndugu, jamaa na marafiki zake wengi
walivyodhani.
Aliongeza kuwa anaamini kutokufungwa kwa
ndoa yake kuna sababu ambazo Mungu mwenyewe anazijua na wala hawezi
kumlaumu mtu au kulaani chochote kilichoingilia kati kufungwa kwa ndoa
hiyo.
Kuhusu maandalizi ya harusi, alisema
mipango mingi ilishafanyika na baadhi ya fedha zililipwa, lakini
majadiliano yanafanyika kama waliokwishalipwa wanaweza kurudisha angalau
nusu ya fedha.
Alisema baadhi ya fedha zilishalipwa kwa mpambaji, mpishi na mavazi ya harusi lakini ukumbi na vinywaji havikuwa vimelipiwa.
0 comments:
Post a Comment